Mtu kuwa na afya njema siyo jambo linaloweza kuja lenyewe bila wewe mwenyewe kufanya jitihada za kupata maarifa ya kutambua mahitaji ya mwili wako, halikadhalika, kuwa na afya mbaya hakuji kwenyewe, bali huwa ni matokeo ya kutokuzingatia au kutokujua mahitaji ya mwili wako jana, hasa katika suala zima la chakula na mtindo wa maisha unayoishi.
Katika makala ya leo, tutakupa baadhi ya dondoo muhimu zitakazokusaidia kukupa mwanga wa njia bora ya kuishi maisha yenye afya njema kwa kujua hulka ya mwili wako na kufanya kile mwili unataka;
MWILI IMARA
Mwili umetengenezwa ili kufanyakazi na kujishughulisha nyakati za mchana na kupumzika usiku giza linapoingia, ndivyo mwili ulivyoumbwa na ulivyozoea. Ingawa kuna mwanga wa bandia unaoweza kubadilisha usiku ukaonekana kama mchana, lakini viungo ndani ya mwili vinafuata asili yake na huwezi kuvidanya.
Hivyo huna haja ya kushindana na mwili wako, kama una uhuru wa kupanga muda wako, ni vyema kufanyakazi zako mchana na kisha ukalala mapema na kuamka mapema. Hii itaupa mwili nafasi ya kutosha ya kupumzika wakati nishati yake inapokuwa katika kiwango chake cha chini. Utashangaa kiwango cha kazi au michezo utakayoweza kuifanya kwa kuamka asubuhi mapema.
Hapa inasisitizwa kwamba kulala na kuamka mapema ndiyo mwili unavyotaka na ndivyo ambavyo utakavyoweza kufanya kazi au shughuli yako yoyote kwa ufanisi zaidi na bila kuuchokesha mwili.
TIBA MBADALA
Vyakula kama vile matunda, mboga na baadhi ya vyakula vingine vilivyopo jikoni kwako, vina uwezo mkubwa wa kutumika kama tiba mbadala. Ni vizuri kujua uwezo wa kila tunda, mboga au mmea wowote katika kutibu magonjwa madogo madogo kama kichwa, tumbo, mafua, n.k, badala ya kukimbilia matumizi ya dawa kali kali (Anti Biotic).
Ukila matunda na mboga mboga na chakula chenye mlinganyo (balanced diet) unajiwekea kinga katika mwili wako na itakukinga na magonjwa mbalimbali yasiyo ya lazima.
0 comments:
Post a Comment